​SERIKALI YASISITIZA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA HAKI ZA WANYAMA

Imewekwa: Wednesday 01, December 2021

Serikali imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa haki za wanyama ambazo zimeonekana kukiukwa kwa kiasi kikubwa siku za hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za ukaguzi na ustawi wa wanyama nchini Dkt. Annette Kitambi wakati atoa elimu kuhusiana na sheria na kanuni mbalimbali zinazolinda haki za wanyama wanaofugwa nchini kwenye maonesho ya Siku ya Mbwa yaliyofanyika leo (27.11.2021) Viwanja vya Gymkhana mkoani Morogoro

“Kwanza kabisa sheria inasema mnyama ana haki ya kutunzwa hivyo mfugaji anawajibika kumtunza vizuri mnyama wake ikiwa ni pamoja na kumpa chakula kizuri, banda ambalo litamkinga dhidi ya mvua na jua na liwe zuri lenye mwanga wa kutosha kwa sababu wengi huwa tunajisahau na kuweka mabanda yenye giza” Amesisitiza Dkt. Kitambi.

Dkt. Kitambi amebainisha kuwa wanyama wana haki ya kisheria ya kutibiwa kama anavyotibiwa binadamu ambapo amesisitiza kuwa mfugaji ana wajibu wa kumpeleka mnyama kwa daktari wa mifugo ili aweze kupatiwa matibabu na kufuata maelekezo yote yatakayotolewa na mtaalam wakati wote wa matibabu hayo.

“Lakini jambo jingine pale utakapoona mbwa anateseka mahali, sheria inakuruhusu umtaarifu kiongozi wa lile eneo ili akupe kibali cha kumchukua na kumtunza mbwa huyo ambapo mmiliki wake atakamatwa na kurejesha gharama zote za matunzo ikiwa atahitaji kumchukua tena mbwa wake” Ameongeza Dkt. Kitambi.

Dkt. Kitambi amesema kuwa changamoto inayowakabili wafugaji wa wanyama mbalimbali kwa hivi sasa ni usugu wa vimelea ambao unatokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa wakati wa kuogesha mifugo au kutumia madawa yasiyostahili kuogeshea mifugo hiyo.

“ Mtu unaambiwa uchanganye CC 20 za dawa wewe kwa sababu unaona ni gharama unachanganya CC 10, kupe anaweza akatoka lakini ukiogesha tena wakati mwingine utakuta wale kupe wameshajenga usugu hivyo ninawaomba wafugaji kote nchini fuateni maelekezo yanayotolewa na wataalam tena wale waliosajiliwa na Serikali kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo” Amesema Dkt. Kitambi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mrakibu wa Polisi Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Morgan Marunda amewapongeza wadau wa mbwa mkoani Morogoro kwa kuandaa maonesho hayo ambapo amewataka wananchi kutumia maonesho hayo kujifunza namna wanavyoweza kutumia mbwa kwa ajili ya kulinda usalama wao na mali zao.

“Kwetu sisi jeshi la Polisi, Mbwa ni nyenzo muhimu katika suala zima la ulinzi na usalama wa raia na mali zao na ndio maana tunao mbwa wenye uwezo wa kufanya mambo mbalimbali hivyo ninatoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanafuga mbwa na kuwapa mahitaji yao yote ya msingi ikiwa ni pamoja na mafunzo yatakayowawezesha kuwasaidia kuwalinda” Amesema Marunda.

Maonesho ya Mbwa mkoani Morogoro mwaka huu yameandaliwa na Chama cha wadau wa Mbwa mkoani humo (MCA) ambapo yamelenga kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi mbalimbali ya mnyama huyo na namna anavyotakiwa kutunzwa ili aweze kuleta tija kwa jamii.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022