​SERIKALI KUKUZA SEKTA YA UVUVI KUPITIA ZANA BORA

Imewekwa: Tuesday 28, September 2021

Serikali imesema imedhamiria kuendeleza sekta ya uvuvi nchini kwa kuhakikisha inanunua zana bora za uvuvi kwa ajili ya wavuvi ili shughuli za uvuvi ziwe endelevu na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amebainisha hayo leo (10.09.2021) katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi injini sita za kupachika kwenye boti kwa ajili ya vyama sita vya ushirika wa wavuvi na kubainisha kuwa nia ya serikali ni kuona mchango wa pato la taifa katika sekta ya uvuvi unakua kwa kujenga mazingira mazuri ya kuvua rasilimali za uvuvi zilizopo nchini.

Mhe. Ndaki amesema injini hizo zenye thamani ya Shilingi Milioni 58.7 zilizogaiwa kwa vyama vya Kabwe kilichopo Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa, Mwamgongo Wilaya ya Kigoma Vijijini Mkoani Kigoma, Msanda Mkuu Wilaya ya Mtwara Vijijini Mkoani Mtwara, Kilwa Kivinje Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi na Igombe Wilaya ya Ilemela pamoja na Chembaya kilichopo Wilaya ya Bushosa Mkoani Mwanza, ni sehemu ya fedha iliyoidhinishwa na serikali kwa ajili kuwasaidia wavuvi.

“Kwa mwaka jana na mwaka huu serikali imetenga Shilingi Milioni 200 ya kununua vifaa na zana mbalimbali za uvuvi kwa ajili ya wavuvi.” Amesema Mhe. Ndaki

Katika kuhakikisha wavuvi wanaendelea kupata misaada mbalimbali kutoka serikalini, amewaasa wajiunge kwenye vyama vya ushirika wa wavuvi vinavyotambulika kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na taifa na kazi zao ziwe zinafanyika kwa kufuata utaratibu unaoeleweka.

Aidha, amewataka wavuvi kuelimisha wenzao kutoendeleza uvuvi haramu kwa kuwa uvuvi huo hauna tija yoyote na husababisha madhara kwa mazalia ya samaki pamoja na kuharibu shughuli za uvuvi endelevu.

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ametoa rai kwa wadau wa sekta ya uvuvi nchini kuwa, zoezi la kukabidhi injini hizo za kupachika kwenye boti liwe chachu ya wao kujipanga vyema kwa kuwa fursa zipo nyingi katika sekta hiyo.

Mhe. Ulega amewataka wadau hao kuhakikisha vyama vyao vya ushirika wa wavuvi vinakuwa imara na vifanye kazi kwa kufuata utaratibu na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha wavuvi wanainuka na kuchangia zaidi katika pato la taifa kupitia sekta ya uvuvi nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema wizara imekuwa ikitoa injini hizo mara kwa mara kwa vyama vya ushirika wa wavuvi ambavyo vimesajiliwa na kutambuliwa kisheria pindi inapopata fedha.

Pia, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikitumia vigezo mbalimbali kwa vyama vya ushrikia vya wavuvi kupata injini za boti, kikiwemo cha ushiriki wao katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi na kufafanua kuwa vyama hivyo sita vimekidhi kigezo hicho kwa kuwa wamekuwa wakishirikiana na wizara katika kupiga vita uvuvi haramu.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge kutoka kwenye majimbo yaliyotoa vyama sita vya ushirika wa wavuvi, vilivyokabidhiwa injini za kupachika kwenye boti, Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula ametaka kuwepo kwa elimu zaidi kwa kulinda maeneo yanye mazalia ya samaki na kuwepo uvuaji wa samaki kwa vipindi.

Dkt. Mabula amesema kwa sasa wavuvi wamekuwa wameelewa juu ya uvuvi haramu hivyo ni vyema kulinda na kusimamia maeneo ya mazalia ya samaki kutovamiwa na wavuvi na kuharibu uendelevu wa uvuvi katika maeneo yao.

.