SERIKALI KUHIMILISHA NG’OMBE MIL. 5 IFIKAPO 2025.

Imewekwa: Wednesday 01, September 2021

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta yake ya Mifugo ipo mbioni kununua kiwango kikubwa cha gesi aina ya “liquid nitrogen” kutoka kiwanda cha kutengenezea gesi hiyo kinachojulikana kama “Tanzania Oxygen Limited” (TOL)kilichopo Mkoani Dar-es-salaam.

Hayo yamesemwa leo (17.08.2021) na kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Mifugo) Dkt. Bedan Masuruli mara baada ya kutembelea kiwandani hapo ili kukagua uwezo wa kuzalisha gesi hiyo ambapo ameridhishwa na kiwango cha uzalishaji kilichopo na kuahidi kuanza mchakato wa taratibu za manunuzi ya gesi hiyo.

“Waziri wetu Mhe. Mashimba Ndaki ametuagiza tuhakikishe tunahimilisha ng’ombe milioni 5 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa na jambo hilo haliwezi kufanikiwa kama hatutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa gesi hii kwa sababu ndio inayotumika kuhifadhi mbegu hivyo baada ya kuwatembelea leo tumeridhika na kiwango chao cha uzalishaji na tuna uhakika kiwango hiki kitatusaidia kufikisha lengo letu” Amesema Dkt. Masuruli.

Dkt. Masuluri ameongeza kuwa lengo la Wizara hiyo ni kuhakikisha inazalisha mbegu bora za ng’ombe wa nyama na maziwa kupitia teknolojia ya uhimilishaji ambapo amewataka wafugaji watarajie kuanza kupata mbegu hizo ili waweze kufanya shughuli yao ya ufugaji kwa tija.

Akibainisha mabadiliko chanya yatakayopatikana baada ya kuanza matumizi ya gesi kutoka kiwandani hapo, Meneja wa kituo cha Uhimilishaji cha Sao-Hill kilichopo Mji mdogo wa Mafinga, Thomas Tegulo amesema kuwa itawasaidia kuhimilisha ng’ombe wengi zaidi tofauti na ilivyo hivi sasa kutokana na mitambo ya kutengenezea gesi hiyo iliyopo kituoni hapo kuharibika.

“Mtambo wetu wa kuzalisha gesi ya “liquid Nitrogen” umeharibika kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa hivyo tumefarijika kuona kiwango kikubwa cha uzalishaji wa gesi hiyo kilichopo hapa ambapo sasa tuna uhakika tutazalisha mitamba bora mingi zaidi” Amesema Tegulo.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na biashara wa kiwanda hicho Mhandisi Daudi Mlwale amesema kuwa kiwanda chao kimesimika mtambo mkubwa zaidi wa kuzalisha gesi hiyo ambao una uwezo wa kuzalisha wastani wa lita 7200 za gesi hiyo kwa siku.

“Ni faraja kwetu kuona Wizara na Serikali kwa ujumla imeona upo umuhimu wa kununua gesi inayozalishwa hapa nchini na sisi tunawakaribisha na kuahidi kufanya nao kazi kwa sababu uwezo upo na nia ipo kwa hiyo ni suala tu la kukamilisha taratibu chache ili tuweze kuzalisha na kuwapatia” Ameongeza Mhandisi Mlwale.

Kwa kipindi cha miaka mitano ijayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta ya Mifugo imedhamiria kuhimilisha ng’ombe milioni 5 lengo likiwa ni kuhakikisha wafugaji wote nchini wanakuwa na mifugo bora na yenye tija ili kuifanya sekta hiyo kuchangia kikamilifu kwenye pato la taifa.

.