​SERIKALI IMETOA LITA 17,520 ZA DAWA ZA RUZUKU ZA KUOGESHEA MIFUGO

Imewekwa: Monday 03, January 2022

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutekeleza zoezi la ugawaji dawa za kuogeshea mifugo hapa nchini kwa lengo la kuikinga mifugo dhidi ya magonjwa yaenezwayo na kupe na ndorobo.

Akizungumza leo (22.12.2021) wakati wa kukabidhi dawa hizo kwenye mkoa wa Songwe, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga amesema kuwa wizara ina utaratibu wa kutoa madawa za ruzuku kwa ajili ya kudhibiti magonjwa.

Prof. Nonga amesema kuwa kwa mwaka huu wa fedha wizara imetoa jumla ya lita 17,520 za dawa za ruzuku za kuogeshea mifugo kwa mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo kwa mkoa wa Songwe wamepatiwa lita 260. Lengo la wizara ni kuhakikisha inadhibiti magonjwa ya mifugo yaenezwayo na kupe na ndorobo hivyo kuwahakikishia wafanyabiashara na watumiaji wa mazao ya mifugo usalama wa chakula.

Akizungumza baada ya kupokea madawa hayo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Omary Mgumba ameishukuru wizara kwa kuamua kutoa madawa hayo ya ruzuku kwani yatawasaidia wafugaji ambao wamekuwa wakilalamika kuwa hawapati madawa.

Pia ameishauri wizara kuhakikisha wanawatambua wauzaji wa madawa katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha wafugaji waliopo vijijini wanawatambua ili iwe rahisi kwa wafugaji kuwafikia pale wanapokuwa wanahitaji kununua madawa. Aidha, ameipongeza wizara kwa uamuzi wa kutoa madawa ya ruzuku na kwamba watahakikisha kuwa madawa hayo yatakwenda kutumika kama ilivyokusudiwa.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022