NARCO YAELEKEZWA KUIPATIA KITALU KAMPUNI YA CHOBO

Imewekwa: Wednesday 28, July 2021

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuipatia Kampuni ya Chobo Kitalu Mbadala katika eneo la Mradi wa Mwisa II lililopo Wilayani Muleba, Mkoani Kagera baada ya kuchelewa kuendeleza Kitalu cha awali alichopewa katika Ranchi ya Mabale na kupelekea wawekezaji wengine kutumia eneo hilo.

Ndaki alitoa agizo hilo alipokutana na mwekezaji huyo jijini Dodoma Julai 27, 2021 na kukubaliana kuwa Wizara itampatia eneo lingine katika mradi wa Mwisa II ili aweze kuendeleza uwekezaji katika sekta ya mifugo.

Kufuatia makubaliano hayo, Waziri Ndaki ameielekeza NARCO kushughulikia jambo hilo kwa haraka ili mwekezaji huyo aweze kuendelea na shughuli zake za uwekezaji nchini.

“Kama nilivyosema sisi tuko tayari kushirikiana na Chobo pamoja na wawekezaji wengine kwa lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya mifugo ili kutimiza malengo ya Tanzania ya Viwanda,” alisema Ndaki

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo pamoja na kumshukuru Waziri kwa hatua hiyo, alisema kuwa uamuzi huo utasaidia kiwanda chake kupata malighafi iliyobora kutoka kwa mifugo watakayoiwekeza katika eneo hilo na anaamini kwa ushirikiano wanaopata kutoka kwa NARCO na Wizara wataweza kuzalisha bidhaa bora itakayoweza kushindana katika Soko la Kimataifa.

Aliongeza kuwa kiwanda chake cha kuchakata nyama ni kikubwa na kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 600 na mbuzi 1500 kwa masaa nane, hivyo kupitia uwekezaji huo kampuni yake itaweza kutengeneza mnyororo wa thamani utakaoweza kufaidisha maelfu ya Watanzania.

Julai 9, 2021 Waziri Ndaki alipokuwa katika ziara Mkoani Kagera alimtaka mwekezaji huyo kukubali kuachia Kitalu cha Mabale ili kuepusha mgogoro uliopo baina yake na wawekezaji wengine ambao wanatumia eneo hilo alilokabidhiwa awali na kumuahidi kuwa pindi atakapokuwa tayari kuwekeza Wizara itampatia eneo lingine ambalo litakuwa zuri zaidi kwa uwekezaji wake.

.