NAIC YATAKIWA KUFIKIA LENGO LA KUHIMILISHA NG’OMBE MILIONI 1 KWA MWAKA

Imewekwa: Tuesday 04, January 2022

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amekitaka Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) kilichopo Mkoani Arusha kuhakikisha wanafikia lengo la kuhimilisha Ng’ombe Milioni 1 kila Mwaka ili ifikapo mwaka 2025 wawe wamefikia lengo la kuhimilishaNg’ombe Milioni 5.

Waziri Ndaki alitoa maelekezo hayo Disemba 29, 2021 wakati akikabidhi Basi jipya aina ya TATA kwa Uongozi wa kituo hicho ili waweze kulitumia katika shughuli zao za kila siku ikiwemo mafunzo kwa vitendo na kuwasambaza Wataalamu katika Kambi mbalimbali za Uhimilishaji.

“Niwatake NAIC na Wataalamu waliofundishwa kuhimilisha wahakikishe tunahimilisha ng’ombe milioni moja kama ambavyo lengo letu linavyotutaka kwa mwaka huu, na usafiri huu tunaowakabidhi leo utusaidie kufikia lengo hilo”, alisema Mhe. Ndaki

Awali, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Bedan Masuruli alisema kuwa Wizara ilitenga kiasi cha shilingi Milioni 100 kwa ajili ya kununua Basi hilo ambalo wanatarajia litasaidia kituo cha NAIC kufanya shughuli zao za mafunzo kwa vitendo na kuwapeleka kwa wakati Wataalamu katika Kambi za Uhimilishaji.

Naye, Kaimu Mkurugenzi, Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), Dkt. Dafay Bura aliishukuru Serikali kwa kuwapatia Basi hilo huku akisema kuwa litawasaidia kutatua kero ya muda mrefu waliyokuwa nayo ya ukosefu wa usafiri, na kuahidi kwamba watalitunza na kulitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022