​MATOKEO YA UTAFITI ZIWA TANGANYIKA YAWEKWA WAZI

Imewekwa: Wednesday 01, September 2021

Shirika la Chakula na Kilimo ulimwenguni (FAO) kupitia mradi wake wa “FISH4ACP” leo (25.08.2021) limewasilisha matokeo ya utafiti ambao lilifanya kuhusiana na uvuvi wa Ziwa Tanganyika.

Matokeo ya utafiti huo ambao ulilenga kutathmini mnyororo wa thamani uliopo kwenye shughuli za Uvuvi zinazofanyika Ziwa Tanganyika yameonesha kukua kwa Uvuvi wa Ziwa Tanganyika huku pia yakibainisha uwepo wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wavuvi na kusababisha wasifikie malengo yao kwa wakati.

Akizungumza mara baada ya kupokea matokeo hayo ya Utafiti, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji Dkt. Nazael Madala ambaye pia alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) katika warsha hiyo amesema kuwa hatua inayofuata ni Wizara yake kwenda kufanyia kazi yote yaliyobainishwa kwenye taarifa hiyo ili kuhakikisha Wavuvi wa Ziwa Tanganyika wananufaika ipasavyo kutokana na kazi zao.

“Miongoni mwa yale yaliyobainishwa kwenye matokeo hayo ni ukosefu wa mitaji kwa wavuvi wadogo hivyo tutahamasisha wavuvi kujiunga kwenye vikundi kisha tutawasiliana na wataalam wetu wa Dawati la Sekta binafsi ili waweze kuwatafutia mitaji wavuvi hao” Amesema Dkt. Madala.

Katika hatua nyingine Dkt. Madala amewataka wavuvi hao kuachana na uvuvi haramu ili waweze kunufaika na rasilimali za Ziwa Tanganyika kwa muda mrefu zaidi.

“Utekelezaji wa matokeo ya utafiti huu hauwezi kufanyika kama wavuvi wa Ziwa Tanganyika wataendelea na shughuli za uvuvi haramu na hata hii miradi inayohakikisha wavuvi wananufaika kutokana na shughuli hii haitokuwepo tena” Amesisitiza Dkt. Madala.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) Dkt. Ismail Kimirei amesema kuwa matokeo ya utafiti huo yanatokana na kazi ya muda mrefu ambayo taasisi yake iliifanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi kwa upande wa Ziwa Tanganyika ili yaweze kuendana na mahitaji ya wahusika.

“Sasa leo ndo tumewaita wadau hawa ambao taarifa zote zilitoka kwao ili wasikie na kupitisha matokeo ya utafiti huo na hatimaye uanze kutekelezwa na mamlaka zinazohusika,” Amesema Dkt. Kimirei.

Kwa upande wake mmoja wa wavuvi wa Ziwa Tanganyika, Suzan Ezekiel amesema kuwa matokeo ya utafiti huo yatawasaidia kupata suluhisho la changamoto ya uvuvi wa msimu ambao umekuwa maarufu kwa upande wa Ziwa hilo.

“Kuna msimu mvuvi wa Ziwa Tanganyika huwa hana hata fedha ya kujikimu kwa sababu hana uvuvi endelevu” Amesema Suzan.

Mradi wa “FISH4ACP unalenga kuboresha hali ya Uvuvi wa ziwa Tanganyika kwa kipindi chote cha utekelezaji wake hadi mwaka 2024.

.