MAJALIWA ATOA MAELEKEZO 10 KUBORESHA SEKTA YA MIFUGO

Imewekwa: Tuesday 28, September 2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema kuwa pamoja na Serikali kuhakikisha ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza sekta ya mifugo unakuwa mkubwa, bado kuna haja ya kuboresha maeneo kadhaa ili sekta hiyo iweze kuchangia kwa kiasi kikubwa katika adhma ya Serikali kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Majaliwa alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo uliofanyika Mkoani Dar es salaam Septemba 7, 2021 huku akitoa maagizo 10 kwa lengo la kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelezwa kikamilifu.

Akiwa katika mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa aliziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatekeleza Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2002 kwa kutenga asilimia 15 ya mapato yatokanayo na mifugo na kuwekeza katika Sekta ya Mifugo.

Pili aliwataka Viongozi na Watendaji wa Serikali, kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na sekta binafsi wakiwemo wafugaji katika kuwawezesha kuwekeza na kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo majosho, malambo visima vya maji na maeneo ya malisho.

Aliongeza kuwa Mamlaka za Serikali za Mtaa zihakikishe zinashirikiana na wadau wa sekta binafsi wakiwemo wafugaji katika kutenga, kupima, kusimamia na kuendeleza maeneo ya malisho.

Aliendelea kuitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhamasisha wafugaji kuboresha mifugo yao ili kuongeza tija katika uzalishaji kupitia uhimilishaji, upandishaji wa madume na mitamba bora.

Aidha, Waziri Mkuu huyo aliiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi iimarishe Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) kwa kuboresha miundombinu na kupatiwa fedha za kufanya tafiti zenye tija kwa sekta ya mifugo huku akisisitiza kuwa mahusiano ya kitaalamu baina ya Taasisi ya Utafiti na Wafugaji yaimarishwe ili kuwezesha matokeo ya tafiti zenye mafanikio katika sekta ya mifugo kutumika na wafugaji na kuleta tija.

Aliendelea kusisitiza kuwa uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za mifugo uimarishwe ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo sambamba na kuwahamasisha wafugaji kutumia mifugo bora iliyofanyiwa utafiti na kuonesha kuwa na tija aidi huku akiongeza kuwa Taasisi zinazozalisha mbegu bora za mifugo ziimarishwe ili ziweze kuzalisha na kugawa mbegu hizo zenye ubora kwa wafugaji.

Majaliwa alisema kuwa ili sekta ya mifugo iwe na tija ni muhimu huduma za ugani ziendelee kuimarishwa ili wafugaji wapate mbinu bora za ufugaji sanjari na kuimarisha masoko ya mifugo ili wafugaji waweze kuuza mifugo yao kwa bei nzuri.

Aliongeza kwa kusisitiza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ishiriki kikamilifu katika kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi huku akitaka ihakikishe wafugaji wanaelimishwa na kuhamasishwa kufuga kulingana na maeneo waliyonayo.

Waziri Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kuagiza kuimarishwa kwa Vyama vya ushirika katika sekta ya mifugo ili vitumike katika kutafuta masoko na kutatua changamoto za wafugaji kwa pamoja.

Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema kuwa wizara yake kwa kushirikiana na wadau wameanza kampeni ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji ambayo ni takwa la kisheria kulingana na sheria ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji ya mwaka 2010 kwa kutumia njia ya hereni.

.