​DKT. MPANGO ATAKA VYOMBO VYA HABARI KUSAMBAZA ELIMU YA UFUGAJI BORA

Imewekwa: Wednesday 03, August 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amevitaka vyombo vya habari nchini kusambaza elimu juu ya ufugaji bora wenye tija kwa wafugaji ili kujikwamua kiuchumi.

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango amebainisha hayo (01.08.2022) jijini Mbeya wakati akifungua rasmi Maonesho ya Wakulima Kitaifa (Nanenane) kwa Mwaka 2022 katika viwanja vya John Mwakangale, ambapo amesema ni wakati ambapo vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kujikita zaidi katika kutoa taarifa juu ya elimu ya ufugaji bora pamoja na wataalamu kutembelea wafugaji.

“Lazima tuwe na vipindi vya elimu kwa ajili ya wakulima na wafugaji wa aina zote ili wananchi waelewe namna ya ufugaji bora na faida nyingi wazipatazo.” Amesema Mhe. Dkt. Mpango

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango akizungumza zaidi wakati akitembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa mwaka 2022 yenye kauli mbiu, Kilimo ni Biashara, Shiriki, Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ametaka maboresho makubwa katika Sekta za Mifugo na Uvuvi na kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa karibu zaidi na wafugaji katika kuwapatia elimu katika tasnia hizo.

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amemuhakikishia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango kwamba wizara inajikita zaidi katika kuhakikisha inazidi kuboreshwa na kutolewa elimu zaidi kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi ili kuongeza tija katika sekta hizo ikiwemo ya uzalishaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo na ukuzaji wa wingi wa vifaranga vya samaki.

Waziri Ndaki amesema wizara imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inaboresha sekta za mifugo na uvuvi na kwamba iko kwenye mipango ya kuanzisha mashamba darasa ya malisho bora ya mifugo katika halmashauri zote nchini ili wananchi waweze kujifunza na kuwa na mashamba bora ya malisho ya mifugo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amemuarifu Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango kuwa tayari bandari ya uvuvi inayojengwa katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ipo katika hatua za awali kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi huo ambao utaimarisha Sekta ya Uvuvi.

Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa Wizara inaweka kipaumbele katika kuhakikisha inaweka mkazo zaidi kwenye uchumi wa buluu ili nchi iweze kunufaika zaidi na mazao ya uvuvi kutoka bahari kuu.

Baadhi ya wadau wa sekta za mifugo na uvuvi walioshiriki katika ufunguzi rasmi wa maonesho hayo wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa juhudi mbalimbali za kuhakikisha sekta hizo mbili zinakuwa huku wakiiomba serikali kuongeza wigo zaidi wa wataalam wa sekta hizo kuwatembelea wadau wake kwa ajili ya kuwapatia elimu.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022