Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
​BUCHA ZA NYAMA, MINADA YA MIFUGO SASA KUWAHI ZAIDI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameagiza bucha za nyama za Serikali zilizopo chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kufunguliwa saa 12 kamili asubuhi na minada yote ya mifugo iliyopo nchini kufunguliwa kuanzia saa 11 alfajiri ili kuwapa fursa wananchi kupata huduma ya kununua mifugo na nyama mapema.
Mhe. Ulega ameyasema hayo kwenye kikao cha Kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kilichokuwa kikijadili utendaji wa kampuni hiyo na Bodi ya Nyama nchini kilichofanyika leo (17.01.2023) kwenye moja ya kumbi za bunge zilizopo jijini Dodoma.
"Utamaduni wetu tumezoea bucha zinafunguliwa alfajiri kwa sababu nyama tunayonunua inatakiwa kuliwa saa 7 mchana, sasa ukifungua bucha saa 4 asubuhi unataka kumuuzia nani? "Amehoji Mhe. Ulega.
Aidha Mhe. Ulega amebainisha kuwa minada mingi ya mifugo nchini ilikuwa ikianza saa 1 asubuhi ili kuwapa fursa wakaguzi wa mifugo kuweza kuiona mifugo hiyo vizuri ambapo kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya nishati ya umeme kwenye minada mingi iliyopo nchini ukiwemo mnada wa Pugu ameagiza minada hiyo kuanza saa 11 alfajiri.
"Mtu anaenda mnadani saa 10 alfajiri kununua mbuzi wawili au watatu kwa ajili ya nyama choma au supu ya wateja wake anamsubiri Afisa wa serikali ambaye anafika saa 1 asubuhi, hakuwezi kufanyika biashara katika mazingira ya aina hiyo" Amesisitiza Mhe. Ulega.
Akizungumzia kuhusu hatua mbalimbali za kuiboresha Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa changamoto kubwa inayoikabili Taasisi hiyo ni ukosefu wa mtaji ambapo mpaka sasa makadirio ya kiasi kinachohitajika ni takribani Bilioni 440 ambazo zinapaswa kutumika kwenye uhuishaji wa miundombinu mbalimbali.
"Moja ni lazima tuhuishe miundombinu ya ufugaji na uanzishwaji wa skimu za unenepeshaji wa mifugo zenye miundombinu yote inayopaswa kutumika kwenye mnyororo mzima wa kuanzia kwenye unenepeshaji mpaka masoko ya mifugo hiyo" Ameongeza Nzunda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma mbali na kuipongeza Wizara kwa Taarifa waliyowasilisha, amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kutoa elimu ya uvunaji wa mifugo na kuitunza vizuri ili iweze kuwa na tija kwa mfugaji na Taifa kwa ujumla.