Home » Latest News » Waziri Mpina akivishwa skafu na vijana wa Skauti wa Wilaya ya Itilima baada ya kuwasili wilayani kushiriki zoezi la upigaji chapa mifugo.

Waziri Mpina akivishwa skafu na vijana wa Skauti wa Wilaya ya Itilima baada ya kuwasili wilayani kushiriki zoezi la upigaji chapa mifugo.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina ameongeza muda wa mwezi mmoja zoezi la upigaji chapa mifugo kitaifa hadi Januari 31 mwaka huu huku akitangaza kuwavua nyadhifa zao Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Erastus Mosha na Kaimu Mkurugenzi wa Ugani na Usajili, Bezia Rwengozibwa kwa kushindwa kusimamia kimamilifu zoezi hilo.

Mbali na wakurugenzi hao pia Maafisa wawili wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Luzangi Deogratius na Felista Kimario wamepewa onyo kali kwa kushindwa kusimamia zoezi hilo la upigaji chapa kitaifa huku waliovuliwa madaraka akiagiza wachukuliwe hatua kali za kinidhamu.

Akizungumza jana katika zoezi la kuhitimisha upigaji chapa kitaifa katika Kijiji cha Migato Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Waziri Mpina alisema kutokana utekelezaji wa zoezi hilo kutokuwa wa kuridhisha kwani asilimia 38.5 ya ng’ombe milioni 19,219,487 waliotakiwa kupigwa chapa ni ng’ombe Milioni 7,401,661 tu ndio waliopigwa chapa tangu Disemba 14, 2016 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipoielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kusimamia zoezi la upigaji chapa mifugo yote nchini.

Mpina alisema hadi kufikia Disemba 31 jumla ya ng’ombe Milioni 7,401,661 sawa na asilimia 38.5 ndio waliopigwa chapa ambapo kiasi cha sh. bilioni 3.7 kwa malipo ya sh. 500 kwa kila ng’ombe zilikusanywa huku Halmashauri 62 zikiwa zimepiga chapa kati ya asilimia 50 na 100, Halmashauri 43 wamepiga chapa kati ya asilimia 10 hadi 50, Halmashauri 23 wamepiga chapa chini ya asilimia 10 huku Halmashauri 30 zikiwa hazijaanza kabisa utekelezaji wa zoezi hilo jambo ambalo amelitafsiri kama ni uzembe, kukaidi na kugoma kutekeleza zoezi hilo kulikofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali.

“Mimi Luhaga Joelson Mpina kwa mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya utambuzi, usafiri na ufuatiliaji wa Mifugo namba 12 ya mwaka 2010 na Kanuni zake za mwaka 2011 G.N 362,ninaongeza muda wa kupiga chapa hadi tarehe 31 January 2018 katika kipindi hicho ng’ombe wote wawe wamepigwa chapa ” alisema Mpina.

Alisema kutokana na udhaifu huu halmashauri zote 30 ambazo hazijaanza kabisa kupiga chapa na halmashauri 23 ambazo zipo chini ya asilimia 10 majina ya halmashauri hizo na majina ya viongozi wake nimeyapeleka kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi kwani Serikali haiwezi kukubali mzaha wa aina hiyo katika usimamizi wa maagizo ya viongozi wakuu wa nchi

Aidha Waziri Mpina alitaja changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa zoezi hili ni pamoja na kutambua na kuorodhesha wafugaji na idadi ya mifugo wanayimiliki, uhaba wa fedha wa kutoa elimu ya uhamasishaji na kutengeneza chapa kwa sababu haikuwemo kwenye bajeti 2016/2017, licha ya agizo hili ni la tangu Desemba 2016.

Hivyo Waziri Mpina ameamuru Halmashauri zote zilizotoza kiwango cha juu ya bei elekezi ya sh 500 wawarudishie wafugaji fedha zao haraka kabla hatua zaidi za kinidhamu hazijachukuliwa dhidi yao.

Mbunge wa Itilima, Njalu Daudi Silanga alifikisha malalamiko ya wafugaji wa jimbo hilo ikiwemo kuendelea kunyanyaswa kwa kukamatwa na kupigwa mnada mifugo yao kwa kisingizio cha kuingia kwenye hifadhi jambo ambalo Waziri Mpina alisema katika uongozi wake ndani ya Wizara hiyo halitaendelea tena.