Home » Latest News » Press release

Press release

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TUKIO LA UTEKETEZAJI WA VIFARANGA KWENYE MPAKA WA NAMANGA ARUSHA

Katika kipindi cha kuanzia tarehe 30.10.2017 kumekuwepo na taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu kukamatwa na kuteketezwa vifaranga vya kuku 6,400 katika kituo cha ukaguzi wa mifugo na mazao yake cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la mji mdogo wa Namanga mkoani Arusha. Baada ya kukamata kwa shehena ya vifaranga hao na kubainika kwamba hawakuwa wameingizwa kwa kufuata taratibu za kisheria, Wizara kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya serikali vya ulinzi na usalama pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania waliviteketeza vifaranga hivyo kwa kuvichoma moto. Kitendo hicho kimezua mjadala katika mitandao ya kijamii kuhusu ya hatua zilizochukuliwa.
Kufuatia tukio hilo Wizara inatoa ufafanuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa kama ifuatavyo:
Kufuatia kuzuka kwa ugonjwa hatari wa Mafua Makali ya Ndege (Highly Pathogenic Avian Influenza- HPAI) mwaka 2006 katika maeneo mengi Duniani na kusabisha vifo kwa ndege na binadamu, serikali iliweka karantini ya kuzuia uingizaji wa kuku na bidhaa zitokanazo na kuku nchini. Katika katazo kupitia tangazo lake la tarehe 07 Juni, 2006. Katazo hilo bado halijaondolewa hadi hivi sasa kwa vile ugonjwa huo bado ni tishio katika mataifa mbalimbali na hivi karibuni umeripotiwa kuwepo katika nchi jirani za Uganda na Zimbabwe.
Miongoni mwa majukumu ya msingi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kudhibiti magonjwa ya Mifugo ikiwa ni pamoja na yale yanayoambukiza kutoka kwa mifugo kwenda kwa binadamu. Katika kutekeleza tunatumia sheria za ndani, miongoni mwa sheria hizo ni Magonjwa ya wanyama na kanuni zake za 2007 n1 2010, sheria ya ustawi wa wanyama no 19 ya 2008 na kanuni zake za 2010. Pia inatuma miongozo kutoka mashirika ya kimataifa yakihusisha Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE), Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Biashara Duniani (WTO) na jumuia za kikanda zikiwemo SADC na EAC.
Inapotokea kuwepo kwa mahitaji ya upatikanaji wa vifaranga vya kuku wazazi (parent stock) kwa ajili ya wafugaji wa ndani vibali maalumu huwa vinatolewa baada ya kufanya tathmini ya usalama kutoka kwenye nchi wanaoagizwa. Taarifa ya hali ya kuwepo kwa hatari ya magonjwa yoyote ya mifugo huwa inatolewa kila na Shirika la Afya ya wanyama duniani (OIE) ambalo hutoa vyeti maalum kwa nchi zilizo salama. Kwa mujibu wa katazo hilo; yeyote anayekiuka masharti hayo hatua stahiki huchukuliwa kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo.
Sheria hizo na kanuni zake zimeainisha maeneo maalum kwenye mipaka ya nchi kwa ajili ya kuingiza au kusafirisha mifugo na bidhaa zitokanazo na mifugo. Maeneo hayo ni kama vile viwanja vya ndege, bandari na sehemu za mipakani mwa nchi. (kanuni ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Wanyama na Mazao yake ya mwaka 2007, kifungu 22). Vituo hivi husimamiwa na wataalam wenye fani ya Afya ya Mifugo. Kulingana na Sheria hii na kanuni zake wafanyabiashara wanaosafirisha kutoka au kuingiza nchini mifugo na mazao yake ni lazima wapite katika vituo hivi wakiwa na vibali halali vilivyotolewa na mamlaka husika.
Katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria na kanuni zilizokwishatajwa hapo juu, wataalamu wa wizara waliokuwepo kwenye kituo cha Namanga tarehe 29.10.2017, walikamata vifaranga vya kuku wa mayai 6,400 waliokuwa wakisafirishwa kutoka Kenya kwenye gari aina ya Hiace yenye usajili T 285 BAY bila kuwa na nyaraka stahiki kutoka mamlaka husika.
Wizara kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya ya Longido na idara nyingine zilizoopo kwenye kituo cha Namanga, baada ya kufanyika tathmini ya ukiukwaji wa sheria tajwa hapo juu, ilionekana mwingizaji wa vifaranga hivi amekiuka Sheria ya Magonjwa ya Wanyama namba 17 ya mwaka 2003 na kanuni yake ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Wanyama na Mazao yake ya mwaka 2007. Na hivyo hatua zitachukuliwa ni kukamata na kuharibu kufuatana na vifungu vya 8 (2), 43(a&b) na 31(1) vya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama namba 17 ya mwaka 2003. Kifungu 8(2) kinampa mamlaka mkaguzi wa Serikali kuangamiza mifugo au mazao yake ambayo yanaonekana yanaweza kusababisha usambazaji wa magonjwa.
Vifaranga vyote viliteketezwa kwa kuchomwa moto mbali na hadhara ya watu na kwamba picha zilizosambazwa kwenye mitandao hazikutolewa na wizara hii.
Ni vyema ikaeleweka kwamba ni jukumu la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya serikali kuhakikisha kwamba inachukua hatua stahiki ili kulilinda Taifa na athari za magonjwa yote yanayoathiri wanyama akiwa pamoja na mifugo, binadamu na mazingira. Hivyo wizara inatoa wito kwa wadau wote kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni yakiwemo yafuatayo;-
• Wafanyabiashara kufuata utaratibu wa kutumia vibali halali vinavyotolewa na mamlaka husika katika kusafirisha wanyama, mifugo na mazao yake
• Wafanyabiashara kusafirisha wanyama, mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi kupitia njia na vituo halali vilivyoidhinishwa na Serikali
• Wafanyabiashara wanaoanza kujihusisha na biashara ya wanyama, mifugo na mazao yake kupata taarifa sahihi kutoka kwa maamlaka zote husika
Wizara inasisisitiza wataalam wote wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kusimamia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyoopo sambamba na utoaji elimu kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari katika kutoa elimu husika.
Imetolewa na:

Mhe. Luhaga Mpina,
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
03/11/2017