Home » Latest News » MHE MPINA AVUNJA MKATABA WA MWEKEZAJI MZEMBE KATIKA RANCHI YA KAGOMA

MHE MPINA AVUNJA MKATABA WA MWEKEZAJI MZEMBE KATIKA RANCHI YA KAGOMA

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina akipima urefu wa bwawa la maji ya kunyeshea mifugo katika Ranchi ya Kagoma Mkoani Bukoba

 

 

 

MPINA ABARIKI NARCO KUVUNJA MKATABA WA MWEKEZAJI MZEMBE KATIKA RANCHI YA KAGOMA
Na John Mapepele
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ameridhia maamuzi ya Kampuni ya Ranchi za NARCO kuvunja mkataba baina ya mwekezaji Agri Vision Global Ltd katika Ranchi ya Kagoma mkoani Kagera na kuamuru aondoka mara moja baada ya mwekezaji huyo kushindwa kutekeleza mkataba huo katika kipindi cha miaka mitano.
Waziri Mpina ametoa maelekezo hayo jana alipotembelea Ranchi ya Kagoma kuangalia shughuli mbalimbali katika Ranchi hiyo ambapo ametoa siku saba kwa mwekezaji huyo kuondoka katika eneo hilo na badala yake Serikali kupitia NARCO kuendelea kusimamia shughuli za mifugo katika Ranchi hiyo.
“Ninakuagiza Mkuu wa Wilaya kuanzia sasa hakikisha unaimarisha ulinzi katika ranchi hii katika kipindi cha kukabidhi Ranchi baina ya Serikali na Mwekezaji ili kusitokee hujuma zozote” alisisitiza Mpina
Alitaja baadhi ya mambo ambayo hayakutekelezwa na mwekezaji huyo kuwa ni pamoja na kujenga machinjio ya nyama, kujenga kiwanda, kutoa gawio la shilingi bilioni tatu kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano, kutoa shilingi 2672 kwa hekta moja kama tozo la ardhi na kushindwa kuendeleza miundombinu ya NARCO waliyoikuta wakati wanaingia mikataba hiyo miaka mitano iliyopita.
Waziri Mpina amemuagiza Meneja Mkuu wa NARCO, Profesa Philemoni Wambura kuhakikisha kwamba ndani ya siku saba anamleta Meneja katika Ranchi hiyo kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za ranchi hiyo na kuhakikisha kuwa inafanya kazi zake kisasa.
Aidha Mpina ametoa siku saba kwa Uongozi wa NARCO kuhakikisha kuwa imefanya tathmini ya hasara zilizosababishwa na mwekezaji huyo ili taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi yake ili aweze kuilipa Serikali ikiwa ni pamoja na shilingi bilioni kumi na tano kama gawio la miaka mitano iliyokaa ambalo amesema halijawahi kulipwa hata shilingi moja.
“Sasa tumeamua kuchukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wawekezaji wasiowaaminifu wanaotaka kuihujumu serikali katika sekta hizi za mifugo na Uvuvi” alihoji Mpina
Alionya wawekezaji kuacha tabia ya kuidanganya serikali kwamba wanauwezo wa kuwekeza katika vitalu ili wapewe lakini wanabadili matumizi baada ya kupewa. Aliongeza kwamba Serikali imegundua baadhi ya wawekezaji wanaopewa vitalu wanawakodisha wafugaji kutoka nchi jirani na kujipatia faida wakati Serikali haipati chochote.
Awali, akipewa ripoti ya maendeleo ya mifugo na uvuvi na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Deodatus Kinawiro mbaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba . alisema kutokana na oparesheni za uvuvi haramu zinazoendelea wilaya ya ngara imekamata tani 6 za samaki zilizokuwa zikipelekwa katika nchi ya burundi .